Hoja hiyo imeidhinishwa kwa kura nyingi ambazo ni sawa na asilimia 88 wakati wa Kongamano la Kitaifa la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vya Norway (LO) lililofanyika Oslo, mji mkuu wa nchi hiyo, kuanzia tarehe 8 hadi 9 Mei.
Kamati ya Palestina ya Norway imesema kuwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la nchi hiyo (LO) litaanza kuisusia kiuchumi Israel baada ya kulipigia azimio hilo kura za ndio 240 dhidi ya 69 za hapana.
Azimio hilo linaeleza kuwa: Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vya Norway sasa linautaka Mfuko wa Hazina wa Taifa wa nchi hiyo, makampuni ya ndani na taasisi za fedha kuacha kufanya biashara zote na Israel na zile zinazohusishwa na serikali ya Israel.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepongeza hatua hii kupitia taarifa yake rasmi na kuitaja kuwa ni hatua ya kijasiri na ni ushindi kwa haki za wananchi wa Palestina.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Norway limelitolea wito Shirika la Kazi Duniani (ILO) kufuata mfano huo wa Norway.
Steinar Krogstad, Naibu Mkuu wa muungano huo mkubwa wa Norway amesema muungano huo unashinikiza kuondolewa kiasi cha dola trilioni 1.8 za Norway kwenye makampuni yanayofanya kazi katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu (Israel).
Ameeleza wazi kwamba msimamo wao unakwenda sambamba na kanuni kuu ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la Norway wa kujiepusha kuwekeza katika makampuni yanayokiuka sheria za kimataifa.
342/
Your Comment